Tuesday, November 1, 2011

Amana Hakuna Amani

Ama kwa hakika nina kila sababu ya kusema haya kuhusiana na Hospitali yetu ya Wilaya Ilala, Hospitali yenye majengo mazuri ambayo pia iliwahi kutembelewa na Mheshimiwa Mkubwa Ulimwenguni Bwana Bushi (Hospitali ya AMANA).

Sehemu ya mbele ya Hospitali ya AMANA

Kwa Mtazamo wa haraka unaweza sema kuwa kutokana na uzuri wa majengo yake basi kila namna ya ugonjwa ama mgonjwa utapona/atapona (kama kupona kwa mtu ni majengo) lakini hali halisi ya watenda kazi (Madaktari) si Shwari.

Kwanini nasema si shwari?

Najua kuwa pengine mara nyingi haya hutokea lakini naomba nielezee haya niliyoyaona mimi katika siku hizi za karibuni.

Mke wangu ni mjamzito, ni ujauzito wake wa kwanza hivyo humsumbua kila mara. Siku ya J2 kuamkia J3 hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kuwa alikuwa na maralia hivyo alikuwa anamaumivu makali sana sehemu za kiuno na tumboni pia. pia alikua anatokwa na damu mara kwa mara kama mtu aliye kwenye Hedhi. Tukaenda Hospitali iliyokuwa karibu na mahali tunapoishi (ukonga Madafu) ambako kutokana na hali ya kiuchumi tulishindwa na kushauriwa na mmoja wa madaktari wa pale twende Amana kwa kuwa ni Hospitali ya Serikali tutapata huduma nzuri na kwa gharama tutakayoiweza.

Tumefika Amana mapema tukakuta wakifanya usafi, tukangoja mpaka Daktari akaja tukawa ni wa kwanza kuhudumiwa kwenye majira ya saa 12 hivi. Ile tunaingia kwa Daktari tu na kumweleza tatizo lililotuleta kabla hatujajieleza vyema akatupa jibu lililotushtua. Kiurahisi tu anatwambia eti Mtoto wetu amekufa na tukitaka tumpe shilingi elfu Arobaini na Tano (45,000/=) ili akamsafishe mama yake (Mke wangu) ili kuzuia asipatwe na Kansa ya kizazi. Inauma sana kwa kweli.

Kwakua niliogopa ile hali ya kuambiwa mke wangu anaweza kupatwa na Kansa nikajikuta nikiomba aheri ya pesa hiyo naye bila kuchelewa alikubaliana nami na kuchukua hela niliyokuwa nimebaki nayo ambayo ni Shs. 21,000/=. na kuniahidi kuwa anawacheki wagonjwa wawili tu kisha anakuja kutushughulikia, hivyo tutoke nje mara moja.

Kweli baada ya dakika kadhaa akaja na kutuingiza katika chumba kingine na kumuamuru mke wangu alale ili amfanyie huo usafishaji wake kitu ambacho mke wangu alikipinga vikali kitu kilichosababisha ugomvi mkali kati ya Daktari na mke wangu na mimi nisijue cha kufanya.

maamuzi ya mwisho tuliyofikia ni Daktari kuturudishia pesa yetu na kuamua kwenda kufanya Ultra Sound ili kuhakikisha kama ni kweli yule kiumbe alishakufa au la.

Nikamwomba huyo daktari aniandikie niende kwenye Ultra Sound nasi tukaenda.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania J.K. akimpa mawili matatu aliyekuwa Rais wa Marekani ndugu G. W. Bushi katika hospitali ya Amana. Linaloonekana kwa mbali ni jengo litumikalo kwa X-Ray, Vipimo vya Moyo na Ultra-sound.

Hali tuliyoikuta huko kwa kweli ilitutia hofu kabisa. Ingawa tulikuwa ni watu wa mwanzoni kufika hapo lakini baada ya dakika chache baadae waliongezeka watu na kufikia zaidi ya hamsini na hakuna hata mmoja aliyefanikiwa kuingia kwa daktari katika wakati muafaka. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba hao hao madaktari walikuwa wanawaingiza watu wengine (wenye pesa nyingi) kwa mlango wa panya na kuwaacha wale waliopo kwenye foleni kwa sababu ya vijisenti vyao walivyovitoa (5,500/=).

Wagonjwa baada ya kuona imefika majira ya saa nane mchana na hakuna aitwaye wakaanza kuishiwa na imani na kuamua kupiga kelele ndipo askari walipokuja na kuuliza madaktari kulikoni na kuweka sawa mambo na kuondoka zao wakiamini kuwa pako sawa. Alitoka Daktari mmoja na kuwakemea wagonjwa eti kwa nini wameamua kupiga kelele mpaka askari wamekuja, alidai kuwa lengo la Wagonjwa hao lilikuwa ni kumfukuzisha kazi na kuwaahidi kuwaripua katika vipimo yaani atahakikisha ndani ya nusu saa atakuwa ameshawamaliza wagonjwa wote ambao idadi yao ilishafikia zaidi ya hamsini.

Ni kweli kama alivyowahaidi aliwapitisha wagonjwa hao kwenye Ultra Sound kama chupa za soda kwenye mashine za ujazo na kuhakikisha wameisha ndani ya muda mfupi.

Ndani: Alichokuwa anafanya ndani kwa mujibu wa mke wangu ni kumfokea mgonjwa kwa kumuamrisha alale na kuanza kumpaka mafuta tumboni na kisha kupitisha mashine ya Ultra Sound kama pasi ipitishwavyo kwenye nguo isipokuwa hakurudia kama ambavyo tunafanya kwenye nguo ili kuhakikisha inanyooka. Inasikitisha sana. Alichukua karatasi ya vipimo na kuweka majibu yake ambayo tuliporudi kwa daktari (yule aliyeikosa hela yetu baada ya sisi kukataa kumsafisha mke wangu) majibu yake yalikuwa ni kama ni kulipiza kisasi na si kuhudumia mgonjwa wa kawaida tena. Alisema eti tunamsumbua bure wakati huko tumboni hakuna cha mimba wala nini kuna uvimbe tu. Inauma sana kwa kweli.

Tuliondoka tukiwa na imani kuwa MIMBA kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu bado ipo na mtoto atazaliwa bila wasiwasi wowote na wao kwa kuwa hawana utu mioyoni mwao Mungu atawaadhibu kwa hilo. Baada ya siku kadhaa tukaamua kupima upya na kugundua kuwa mimba bado ipom na ina Afya tele. Na kwa hakika imani na hospitali hiyo imenitoka kabisa.

Naomba nieleweke vyema, sina maana ya kwamba Hospitali ni mbaya La hasha bali hawa madaktari wanaichafua Hospitali yetu kwa tabia zao binafsi za kupenda pesa kuliko utu. Wanaona ni rahisi sana kwao kutoa viumbe vya Mwenyezi Mungu visivyo na Hatia kwa maslahi yao binafsi bila kujali ni muda wa miaka mingapi watu hupoteza katika harakati za kutafuta watoto. Mungu Hapendi.

AMANA JAMANI, HAKUNA AMANA

Sunday, December 26, 2010

Ni ngumu kwangu kusahau siku ambayo mdogo wangu huyu alipozaliwa kwani ninakumbuka vitu vikuu VITATU,

Kwanza: Ilikua ni siku ya pili baada ya X-Mass yaani siku ya BOXING.

Pili: Ilikua ni siku ambayo mmoja wa shangazi zangu ambaye kwa sasa ni marehemu (Mungu amlaze mahala pema peponi, Amin) alipokua anaolewa.

Tatu: Ni siku ambayo mimi na baba tulikua bize Town tukitafuta aina gani ya TV inatufaa, ikumbukwe suala la TV lilikua ni adimu sana TANZANIA. Tulifanikiwa kurudi na TV ya Black n White iliyokua na jumba lenye rangi nyekundu.

HAPPY BIRTHDAY BROO
MUNGU akupe maisha marefu na yenye baraka tele. AMIN.

Monday, December 13, 2010

NJEMBA YABAMBWA IKICHEZA VIDUKU KWENYE DALADALA

Jamani jamani jamani! hivi hii hali itaisha lini? Hivi ni nani wa kulaumiwa katika hili?

Kituo cha daladala Ubungo.

Hapa ni sehemu ambayo daladala nyingi ziendazo sehemu mbalimbali za nje na ndani ya jiji la Dar es Salaam zinapoanzia safari yake. Watu huchukua usafiri wa kuelekea waendako toka hapa na hakuna kati yao atakayejua nini kitatokea ndani ya usafiri  (Daladala) aliouchukua. Jamani ndani ya Daladala kuna mengi mno, kati ya hayo yapo mazuri kwa maana watu tofauti hupata nafasi ya kujadili na mada tofauti zihusuzo jamii na mbalimbali yanayowazunguka. HILI ni moja kati ya mambo mazuri.

Daladala aina ya DCM ikitokea Mbagara kuelekea Kivukoni.

Jambo baya huwa ni pale ambapo mmoja kati ya abiria waliopanda ndani ya daladala hilo anapoamua kuonesha kipaji chake cha kucheza na mifuko ya abiria wengine kana kwamba ana ruhusa ya kufanya hivyo. Usipokua makini utajikuta hata ile nauli uliyotegemea kulipia usafiri huo imechukuliwa na Abiria huyu asiye na wema hata theluthi (KIBAKA).

Abiria wakiwa wamejaa kwenye DCM huku wengine wakiwa wamesimama katika style wanayoiita 'KUPIGA RANGI' 

Kutokana na utofauti wa binadamu katika kukidhi haja zao, kila mmoja na njia tofauti na mwingine katika hili. Kuna watu ambao hupanda madaladala si kwa nia ya kuwahi kazini au kuiba kitu cha mtu mwingine La, Hasha! Wao hupanda Daladala na hasa zilizojaa tu ili waweze kujipa burudani ya KIMWILI. Watu hawa ni maarufu sana kwa jina la 'DUNGADUNGA'

Leo nimepata MOOD ya kuyaandika haya ili kuwatahadharisha watu hasa akina dada juu ya hawa watu. Haya yametokea leo wakti nikitokea nyumbani kwangu kuelekea kazini. Kuna njemba moja almanusura aambulie Kichapo kwa sababu ya kucheza KIDUKU nyumba ya mgongo wa dada fulani aliyekuwemo kwenye daladala tuliyoipanda. Jamaa huyo mtanashati ambaye kwa sura ni mzuri na angeweza kumnasa msichana yeyote ambaye angemtaka ameshindwa kufanya hivyo badala yake ameamua kuwa anamalizia shida zake kwenye madaladala yaliyojaa.

Kisa kilikua kama ifuatavyo: Jamaa amepanda kwenye gari kwa kuikimbilia kwa sababu tayari ilikuwa imeshajaa na abiriria wengi walikua wamesimama. Kwa mwendo wa kutoka Banana hadi maeneo ya TAZARA jamaa alionekana akicheza viduku taratibu kwa kumfuata dada wa watu kila hatua aliyosogea. Kumbe kitendo kile kilishuhudiwa vyema na Kondakta wa daladala hiyo ambaye aliamua kunyamaza kimya, (SIKUJUA aliogopa nini). Mbali na kondakta kuna jamaa mwingine ambaye pia alipata bahati ya kuliona hilo lakini alishindwa kuvimilia na kujikuta akimhoji jamaa kwa ukali kuwa alikuwa anataka nini kwa dada huyo (MDUNGWAJI). Jamaa kwa kujiuma uma alijibu kitu ambacho hakikueleweka kitu ambacho kiliamsha hisia za watu karibu wote kwenye daladala hiyo pamoja yule dada (MDUNGWAJI) mwenyewe ambaye kwa mara ya kwanza alisikika akisema, "mi nimemuona muda mrefu akinifuata fuata huku nyuma ila sikujua alikua anafuata nini", alisema dada huyo huku akiendele kuwa baada ya ahapo alisikia kama aliyeloana sehemu zake za MCHINA. Maneno ya dada huyu yaliamsha hisia za Abiria wengine ambao wengine walimuomba kondakta amlete Jamaa huyo (MDUNGAJI) huku nyuma (tulipokuwa tumekaa sisi) ili naye ADUNGWE.

Kwa bahati nzuri kabla ya maamuzi hayo kufikia muafaka jamaa alishuka maeneo ya MTAVA na kupanda daladala jingine ambayo hatukujua kama aliendelea na VIDUKU ama alikoma.

JAMANI mbona mademu wako wengi VIDUKU kwenye daladala vya nini?

Friday, October 15, 2010

MUNGU AMLAZE MAHALA PEMA PEPONI. AMEN.

Ukweli ni kwamba tulimpenda sana, lakini Muumba alimpenda zaidi na mapenzi yake ni lazima yatimie. Ni miezi miwili sasa tangu amefariki lakini machungu tuliyonayo kwa kuondoka kwake ni makubwa kama vile ametutoka jana. MUNGU amlaze mahala pema peponi mama yangu mpendwa. AMEN.
MAREHEMU MAMA YANGU (BI. HABIBA CHUGULO) WAKATI WA UHAI WAKE

Thursday, July 29, 2010

MIAKA MINNE (4) YA NDOA

Harurururururuuuuuuuuuuu. Nikikumbuka hivi vigeregere huwa nacheka peke yangu yaani siamini kuwa sasa imeshafika miaka MINNE tangu watu wapige Vigeregere hivi kwangu siku nilipokuwa naoa. Naam Leo tarehe 29/07/2010 nimetimiza miaka MINNE tangu nilipopiga goti na kukabidhiwa Bi. Fauzia Edward Chami ambaye kwa sasa anaitwa 'MAMA RAHMARITAH'
Mke wangu Mpenzi Fauzia Chami (MAMA RAHMARITAH)


Ninaamini sio mapenzi yangu wala ya Bi. Fau yaliyosababisha tufike hapa tulipo ama yaliyosababisha tudumu kiasi hiki ambacho si kikubwa sana lakini pia si kidogo kwa maana tumeshuhudia ndoa nyingi zilizofungwa baada yetu zikavunjika ndani ya mwaka ama miezi kadhaa tu, haya yote ni mapenzi ya Muumba afanyaye yote haya ka makusudi yake. Mimi na mke wangu tunasema ALHAMDULILLAH na tunamuomba Mungu atuzidishie miaka ya kuishi pamoja, macho ya husda yasituangukie. Amin.
Mwozeshaji alinikabidhi binti huyu kwa kusema "Nimekuozesha" nami nikajibu "Nimemuoa" wamama wakaitikia kwa vigeregere "Rurururururururuuuuuu"

Friday, July 9, 2010

Rahmaritah!

Little Rita na babake mdogo Ismail (Prince Migo)

Tuesday, September 22, 2009

Tumejifunza nini?


Katika kila jambo ambalo mwana wa Adam analifanya na kwa uwezo wa Rabbana likafanikliwa, basi hakuna buni kwa Mwana wa Adam huyo kumshukuru kwalo.
Naam, Takriban mwezi mzima waumini wa dini ya Kiislam walikuwa katika mfungo mtukufu wa Ramadhani. Mfungo ambao ni mojawapo ya nguzo kuu za Uislam. Kwa mafundisho ya vitabu vitukufu vya Iman ya Kiislam Ramadhan ni Mwezi ambao Mja anatakiwa ajikurubishe kwa Mola wake ili kubata Toba na Msamaha wa dhambi zake. Katika Ibada zote ambazo Watu wameamrishwa kuzifanya, hii imeonekana ni Ibada ya pekee kutoka na watu wengi kuitii na kuifuata. Kitu kinachosababisha hata wasio waumini wa Dini hiyo kuhisi kuwa ]kuna ulazima wao pia kuwa watulivu na wengine kuungana nao katika SWAUM.

Hii inathibitika kwa mifano kadhaa katika jamii ikiwemo kupungua kwa idadi kubwa ya watu waliokuwa wakihudhuria sehemu za starehe na mabaa mbalimbali kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya Mwezi huo (Ramadhani) kuingia na kuwatuliza watu.

Ama kwa hakika Dunia ilikuwa Shwari kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa maasi.

Lakini sasa, Swali linakuja kwetu; TUMEJIFUNZA NINI kutokana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao umetuacha na hautakuja tena mpaka Mwakani ambapo mimi na wewe hatujui kama utatukuta?

Je, kuondoka kwa mwezi iwe ndiyo fursa kwetu kujiunga tena na tabia za kumuhasi Muumba?

Mi nawatakia Maisha mema na ningependa pia kuwaasa ndugu zangu pamoja na kuiasa nafsi yangu juu ya kumcha Mola ambaye uwepo wake ni wa DAIMA na endapo tutarudia matendo maovu ambayo tulikuwa tukiyafanya awali (kabla ya Ramadhani) tutakuwa ni watu ambao tulikuwa tunaiabudu Ramadhani na si Mungu ambaye ameileta Ramadhani ilim iwe Kifutio cha Dhambi zetu.

Nawatakia kila la kheri katika maisha yenu ya kila siku.


PashalOnline