Tuesday, November 1, 2011

Amana Hakuna Amani

Ama kwa hakika nina kila sababu ya kusema haya kuhusiana na Hospitali yetu ya Wilaya Ilala, Hospitali yenye majengo mazuri ambayo pia iliwahi kutembelewa na Mheshimiwa Mkubwa Ulimwenguni Bwana Bushi (Hospitali ya AMANA).

Sehemu ya mbele ya Hospitali ya AMANA

Kwa Mtazamo wa haraka unaweza sema kuwa kutokana na uzuri wa majengo yake basi kila namna ya ugonjwa ama mgonjwa utapona/atapona (kama kupona kwa mtu ni majengo) lakini hali halisi ya watenda kazi (Madaktari) si Shwari.

Kwanini nasema si shwari?

Najua kuwa pengine mara nyingi haya hutokea lakini naomba nielezee haya niliyoyaona mimi katika siku hizi za karibuni.

Mke wangu ni mjamzito, ni ujauzito wake wa kwanza hivyo humsumbua kila mara. Siku ya J2 kuamkia J3 hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kuwa alikuwa na maralia hivyo alikuwa anamaumivu makali sana sehemu za kiuno na tumboni pia. pia alikua anatokwa na damu mara kwa mara kama mtu aliye kwenye Hedhi. Tukaenda Hospitali iliyokuwa karibu na mahali tunapoishi (ukonga Madafu) ambako kutokana na hali ya kiuchumi tulishindwa na kushauriwa na mmoja wa madaktari wa pale twende Amana kwa kuwa ni Hospitali ya Serikali tutapata huduma nzuri na kwa gharama tutakayoiweza.

Tumefika Amana mapema tukakuta wakifanya usafi, tukangoja mpaka Daktari akaja tukawa ni wa kwanza kuhudumiwa kwenye majira ya saa 12 hivi. Ile tunaingia kwa Daktari tu na kumweleza tatizo lililotuleta kabla hatujajieleza vyema akatupa jibu lililotushtua. Kiurahisi tu anatwambia eti Mtoto wetu amekufa na tukitaka tumpe shilingi elfu Arobaini na Tano (45,000/=) ili akamsafishe mama yake (Mke wangu) ili kuzuia asipatwe na Kansa ya kizazi. Inauma sana kwa kweli.

Kwakua niliogopa ile hali ya kuambiwa mke wangu anaweza kupatwa na Kansa nikajikuta nikiomba aheri ya pesa hiyo naye bila kuchelewa alikubaliana nami na kuchukua hela niliyokuwa nimebaki nayo ambayo ni Shs. 21,000/=. na kuniahidi kuwa anawacheki wagonjwa wawili tu kisha anakuja kutushughulikia, hivyo tutoke nje mara moja.

Kweli baada ya dakika kadhaa akaja na kutuingiza katika chumba kingine na kumuamuru mke wangu alale ili amfanyie huo usafishaji wake kitu ambacho mke wangu alikipinga vikali kitu kilichosababisha ugomvi mkali kati ya Daktari na mke wangu na mimi nisijue cha kufanya.

maamuzi ya mwisho tuliyofikia ni Daktari kuturudishia pesa yetu na kuamua kwenda kufanya Ultra Sound ili kuhakikisha kama ni kweli yule kiumbe alishakufa au la.

Nikamwomba huyo daktari aniandikie niende kwenye Ultra Sound nasi tukaenda.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania J.K. akimpa mawili matatu aliyekuwa Rais wa Marekani ndugu G. W. Bushi katika hospitali ya Amana. Linaloonekana kwa mbali ni jengo litumikalo kwa X-Ray, Vipimo vya Moyo na Ultra-sound.

Hali tuliyoikuta huko kwa kweli ilitutia hofu kabisa. Ingawa tulikuwa ni watu wa mwanzoni kufika hapo lakini baada ya dakika chache baadae waliongezeka watu na kufikia zaidi ya hamsini na hakuna hata mmoja aliyefanikiwa kuingia kwa daktari katika wakati muafaka. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba hao hao madaktari walikuwa wanawaingiza watu wengine (wenye pesa nyingi) kwa mlango wa panya na kuwaacha wale waliopo kwenye foleni kwa sababu ya vijisenti vyao walivyovitoa (5,500/=).

Wagonjwa baada ya kuona imefika majira ya saa nane mchana na hakuna aitwaye wakaanza kuishiwa na imani na kuamua kupiga kelele ndipo askari walipokuja na kuuliza madaktari kulikoni na kuweka sawa mambo na kuondoka zao wakiamini kuwa pako sawa. Alitoka Daktari mmoja na kuwakemea wagonjwa eti kwa nini wameamua kupiga kelele mpaka askari wamekuja, alidai kuwa lengo la Wagonjwa hao lilikuwa ni kumfukuzisha kazi na kuwaahidi kuwaripua katika vipimo yaani atahakikisha ndani ya nusu saa atakuwa ameshawamaliza wagonjwa wote ambao idadi yao ilishafikia zaidi ya hamsini.

Ni kweli kama alivyowahaidi aliwapitisha wagonjwa hao kwenye Ultra Sound kama chupa za soda kwenye mashine za ujazo na kuhakikisha wameisha ndani ya muda mfupi.

Ndani: Alichokuwa anafanya ndani kwa mujibu wa mke wangu ni kumfokea mgonjwa kwa kumuamrisha alale na kuanza kumpaka mafuta tumboni na kisha kupitisha mashine ya Ultra Sound kama pasi ipitishwavyo kwenye nguo isipokuwa hakurudia kama ambavyo tunafanya kwenye nguo ili kuhakikisha inanyooka. Inasikitisha sana. Alichukua karatasi ya vipimo na kuweka majibu yake ambayo tuliporudi kwa daktari (yule aliyeikosa hela yetu baada ya sisi kukataa kumsafisha mke wangu) majibu yake yalikuwa ni kama ni kulipiza kisasi na si kuhudumia mgonjwa wa kawaida tena. Alisema eti tunamsumbua bure wakati huko tumboni hakuna cha mimba wala nini kuna uvimbe tu. Inauma sana kwa kweli.

Tuliondoka tukiwa na imani kuwa MIMBA kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu bado ipo na mtoto atazaliwa bila wasiwasi wowote na wao kwa kuwa hawana utu mioyoni mwao Mungu atawaadhibu kwa hilo. Baada ya siku kadhaa tukaamua kupima upya na kugundua kuwa mimba bado ipom na ina Afya tele. Na kwa hakika imani na hospitali hiyo imenitoka kabisa.

Naomba nieleweke vyema, sina maana ya kwamba Hospitali ni mbaya La hasha bali hawa madaktari wanaichafua Hospitali yetu kwa tabia zao binafsi za kupenda pesa kuliko utu. Wanaona ni rahisi sana kwao kutoa viumbe vya Mwenyezi Mungu visivyo na Hatia kwa maslahi yao binafsi bila kujali ni muda wa miaka mingapi watu hupoteza katika harakati za kutafuta watoto. Mungu Hapendi.

AMANA JAMANI, HAKUNA AMANA